Browsing by Author "Chuachua, Rashid"
Now showing 1 - 1 of 1
Results Per Page
Sort Options
Item Falsafa ya riwaya za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi katika muktadha wa epistemolojia ya Kibantu(The University of Dodoma, 2016) Chuachua, RashidTasnifu hii inayoitwa ―Falsafa ya Riwaya za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi katika Muktadha wa Epistemolojia ya Kibantu‖ imechunguza namna maarifa ya Wabantu yanavyojitokeza katika riwaya za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi. Uchunguzi huo umezingatia vipengele mbalimbali kama vile uchawi, tambiko, imani au fikra zao kuhusu roho na kifo, moyo, Mungu, mwanya, uzazi, utoaji majina, uganga na ardhi. Taarifa zilikusanywa kwa njia ya mahojiano, majadiliano katika vikundi, mapitio ya maandiko na ushuhudiaji. Taratibu za ukusanyaji wa data ziliongozwa na mkabala wa kifinomenolojia, wakati uchanganuzi wa taarifa uliongozwa na mkabala wa kiepistemolojia. Finomenolojia ni mkabala maarufu katika utafiti wa kitaamuli; epistemolojia ni mkabala mpya katika uchambuzi wa kazi za fasihi. Matumizi ya mkabala huu yamedhihirisha kuwa Wabantu wana namna yao ya kupata maarifa ambayo ni kupitia kani-uhai toka kwa Mungu wao. Wazee walio hai ndiyo chanzo cha maarifa hapa duniani kwa kuwa wana uwezo wa kuwasiliana na wahenga wao kwa urahisi zaidi. Aidha, kujua kwao kumefungwa kwenye duara linalofanywa na kani-uhai toka kwa Mungu, kuja kwa wahenga, kisha kwa watu walio hai na kurudi tena kwa Mungu. Mungu ndiye chanzo kikuu cha kani-uhai. Aliye nje ya duara hili linaloundwa na kani-uhai, hawezi kuwa na maarifa ya kaida za jamii yake. Kwa Wabantu, maarifa ni kujua asili ya kani-uhai na athari zake. Jambo hili hutokana na uzoefu wa muda mrefu wa kaida za jamii husika; pamoja na kudumisha mila na desturi zinazoimarisha uhusiano uliopo ndani ya duara la maisha. Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa; pamoja na kuyaweka mawazo ya Falsafa za Ulaya na Asia katika maandishi yao, kwa kiasi kikubwa, kazi za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi zinawasilisha maarifa halisi ya Wabantu. Utafiti umebaini kuwa maarifa ya Wabantu yanaegemea katika misingi ya kiontolojia. Hivyo basi, ontolojia ndiyo kiini cha epistemolojia ya Kibantu. Katika kudhihirisha hili, vigezo vinavyotumiwa na Wabantu katika kumbainisha mtu vimewekwa bayana. Utafiti pia umebaini kuwa waandishi hawa wawili hawakumwacha mtu akiwa hewani, bali baada ya kumbainisha kwa mujibu wa maarifa yao, wamemweka katika jamii na kumwonyesha anavyothamini amali za jamii yake. Amali hizo ni za kidini au kiimani, kimaarifa na kimatendo. Aidha, utafiti umebaini kuwa uandishi wao umejiegemeza katika mikondo ya Falsafa ya Kiafrika ya kiethinofilosofia na kihekima kama ilivyoasisiwa na Placid Tempels na Odera Oruka kwa kufuatana. Kwa jumla, maarifa au epistemolojia ya Kibantu yameonekana yakiegemea ontolojia kwa kila kipengele; na hivyo, kani-uhai kuonekana kama mhimili mkuu wa falsafa ya Kibantu. Utafiti ulioizaa tasnifu hii umeonekana kuwa na mchango mkubwa katika eneo la Falsafa ya Kiafrika na ya Kibantu. Kwa maoni na upeo wa mtafiti, yumkini, hii ni Tasnifu ya kwanza nchini Tanzania ya kiwango cha shahada ya uzamivu, iliyochokoza taaluma ya Fasihi kwa mtazamo wa falsafa ya Kibantu kwa kutumia riwaya za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi. Vilevile, ni ya kwanza kuutumia mkabala wa epistemolojia ya Kibantu katika uchanganuzi wa kazi za Fasihi. Nadharia hii mpya iliyoegemea uchambuzi wa fikra za Wabantu inaweza kutumiwa na watafiti wengine. Hali hii itasaidia kutotumia nadharia za kigeni pekee katika kuchunguza fasihi ya Kiswahili, hata kwa mambo yasiyohusiana na mitazamo ya kigeni.