Browsing by Author "Stephano, Rehema"
Now showing 1 - 5 of 5
Results Per Page
Sort Options
Item Ufanisi wa tafsiri za viwandani nchini Tanzania: uchunguzi wa vifungashio vya dawa za binadamu(Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 2020) Stephano, Rehema; Gwajekera, Fidel DassanMakala haya yanahusu tafsiri za vifungashio vya dawa za binadamu. Lengo kuu la kuandika makala haya lilikuwa kuchunguza ufanisi wa tafsiri za vifungashio hivyo. Methodolojia ya utafiti huu imejumuisha upitiaji wa tafsiri na usaili kwa wafamasia na watumiaji wa dawa. Lengo la kuwasaili wafamasia ni kupata taarifa kuhusu dhima ya wamiliki wa viwanda vya dawa kufanya tafsiri. Usaili wa watumiaji wa dawa ulilenga kuangalia tija za tafsiri za vifungishio vya dawa, hasa katika Kiswahili kwa watumiaji hao. Matokeo ya utafiti wetu yanaonesha kuwa ufanisi wa tafsiri hufikiwa pale tafsiri inapokidhi dhima zake. Uchunguzi wa vifungashio vya dawa umeonesha matokeo ya aina mbili ambayo ni kufanikiwa na kutofanikiwa kwa tafsiri katika dhima zake. Kufanikiwa kwa tafsiri katika vifungashio vya dawa za binadamu kumejionesha katika dhima mbalimbali kama vile kufanikisha mawasiliano, kufundisha na kujifunza lugha, pamoja na kupanua soko na kuwapa amani walaji wa bidhaa. Kutofanikiwa kwa tafsiri hizi kumetokana na kasoro kama vile udondoshaji, upotoshaji wa taarifa muhimu na kutozingatia sarufi ya lugha lengwa. Kutokana na kutofanikiwa kwa tafsiri za vifungashio hivyo vya dawa, utafiti huu unapendekeza tafsiri sahihi kuzingatiwa ili kukidhi mawasiliano pamoja na dhima nyingine za tafsiri. Kwa kufanya hivyo, dawa zitaweza kununuliwa na watu wengi zaidi kutokana na kuelewa maelekezo yanayotolewa katika lugha mbalimbali.Item Ukiukwaji wa nadharia tumizi ya uakifishaji katika kazi za kitaaluma za wanafunzi wa shule za msingi Tanzania(Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 2020) Stephano, RehemaMakala haya ni zao la tasnifu ya Stephano (2015) yenye mada ya “Uzingatizi wa Viakifishi katika Uandishi wa Kitaaluma: Mifano kutoka Shule za Msingi Tanzania.” Makala inabainisha misingi mikuu ya Nadharia Tumizi ya Uakifishaji na kuonesha ukiukwaji wake katika nyaraka zinazotumika kufundishia na kujifunzia Kiswahili katika shule za msingi. Data za utafiti huu zimetokana na mapitio ya nyaraka za kufundishia na kujifunzia Kiswahili. Nyaraka hizo ni vitini vya masomo ya wanafunzi wa Darasa la VI na VII, na vitabu vya kiada na viongozi vya walimu Darasa I - VII. Matokeo ya uchunguzi wetu yanaonesha kuwa Nadharia Tumizi ya Uakifishaji haizingatiwi kwa uhakika, hasa katika uandishi wa insha. Ni viakifishi vichache tu, nukta, kiulizo, mshangao (viakifishi vya Safu 1) na mkato (kiakifishi cha Safu 4) ikilinganishwa na idadi inayopendekezwa na nadharia (ambavyo ni viakifishi kumi na vinne), ndivyo vinavyotumika. Zaidi, matokeo yanaonesha kuwa, pamoja na kutumika, viakifishi hivyo havitumiki kwa usahihi. Kwa hiyo, makosa ya kuandika sentensi bebanifu, sentensi tata na vipande sentensi hutokea. Makala yanapendekeza Nadharia Tumizi ya Uakifishaji kuzingatiwa wakati wa kuandika ili kuandika matini zinazoeleweka kwa wasomaji.Item Ukubalifu wa tafsiri za kitamaduni: Mfano wa tafsiri ya filamu ya Yesu kutoka Kiingereza kwenda Kinyaturu(The University of Dar es Salaam, 2023) Stephano, RehemaMakala haya yametathmini ukubalifu wa tafsiri za kitamaduni kwa kujiegemeza katika mswada wa tafsiri ya Filamu ya Yesu kutoka Kiingereza kwenda Kinyaturu. Utafiti uliozaa makala haya yameongozwa na Nadharia ya Skopos ya Hans J. Vermeer (1978) ambayo inazingatia lengo la kutafsiri matini lengwa. Utafiti huo pia umetumia mbinu mbili za kukusanyia data: uchambuzi wa matini na majadiliano ya vikundi lengwa, ambapo waigizaji wa sauti za Filamu ya Yesu ambao ni Wanyaturu tisa (9) wa umri wa miaka 40 - 80 walihusishwa katika majadiliano hayo. Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa kuna vipengele vilivyokubalika kwa wazungumzaji wazawa wa Kinyaturu na vingine havikukubalika. Vipengele vilivyokubalika ni uzingatiaji wa tasifida katika kutafsiri miiko na urejeleaji wa wapendwa, yaani matumizi ya majina yanayosawiri hisia za upendo wakati wa kutafsiri. Vipengele vilivyokataliwa ni maneno yaliyopitwa na wakati, kutafsiri maneno kadhaa kwa kisawe kimoja, kutafsiri neno moja kwa visawe tofauti, na utohozi usio na sababu. Matokeo ya utafiti yameonesha zaidi kuwa utohozi wa maneno ya Kiswahili katika kutafsiri kwenda Kinyaturu unatokana na mtagusano wa Kinyaturu na Kiswahili, ambapo wazungumzaji wa Kinyaturu wanaonekana kuhamia katika Kiswahili na utamaduni wake. Makala haya yanaonesha kuwa utohozi huu ni kinyume na Nadharia ya Skopos ambayo tafsiri imekusudiwa ifanyike kwenda Kinyaturu kwa azma ya kuhifadhi lugha hiyo. Kwa upande wa vipengele ambavyo havikukubalika maboresho yalipendekezwa. Kufuatia matokea haya, makala haya yanapendekeza mfasiri kujua tamaduni za lugha chanzi (LC) na lugha lengwa (LL) kabla ya kufanya tafsiri yoyote ya kitamaduni ili kutoa tafsiri inayokubalika. Aidha, makala inasisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wazungumzaji wazawa wanaoishi eneo inapozungumzwa LL ili kuhakiki na kuiwezesha tafsiri ya kitamaduni kukubalika kwa wahusika.Item Utoshelevu wa Mawasiliano kwa Kiswahili katika Teknolojia ya Sikanu: Uchunguzi Kifani wa WhatsApp.(University of Namibia, 2020) Stephano, RehemaMakala hii inahusu uchunguzi wa utoshelevu wa mawasiliano kwa Kiswahili katika teknolojia ya SIKANU. Uchunguzi umejikita katika programu tumizi ya SIKANU ijulikanayo kwa jina la WhatsApp na simu ya mkononi aina ya Tecno F1 imetumiwa kama uchunguzi kifani. Utafiti umetumia mkabala wa kitaamuli, ambapo maelezo na maelekezo ya Kiswahili yaliyomo katika WhatsApp yamechunguzwa katika kupima utoshelevu wake. Vigezo vilivyotumika kupima utoshelevu wa mawasiliano hayo ni uelewekaji, uwepo wa msamiati katika kamusi za Kiswahili na katika matumizi ya wazungumzaji, ngeli za nomino, mpangilio wa viambishi na wa maneno katika tungo. Uchanganuzi umeonesha kuwa msamiati unaotumika katika WhatsApp, kwa kiasi kikubwa, ni toshelevu kiasi cha kukidhi mawasiliano baina ya watumiaji wake. Kuna msamiati ambao unafahamika na kuzoeleka kwa watumiaji na mwingine ni mapya. Msamiati mpyaItem Uzingatizi wa viakifishi katika uandishi wa kitaaluma: Mifano kutoka shule za msingi Tanzania(The University of Dodoma, 2015) Stephano, RehemaUtafiti huu umechunguza uzingatizi wa viakifishi katika uandishi wa kitaaluma kwa wanafunzi wa Shule za Msingi Tanzania zinazotumia mchepuo wa Kiswahili, hasa kwa kujikita katika mtaala wa Kiswahili. Malengo mahususi yaliyoshughulikiwa na utafiti huu ni matatu. Malengo hayo ni kuchambua viakifishi vinavyotumiwa katika uandishi wa kitaaluma wa wanafunzi wa Shule za Msingi Tanzania, kuchunguza makosa ya uakifishaji yanavyojitokeza katika kazi za wanafunzi wa Shule za Msingi Tanzania na kubainisha sababu mbalimbali za makosa ya uakifishaji kwa wanafunzi wa Shule za Msingi Tanzania. Utafiti huu umetumia mbinu mseto katika kukusanya data. Vilevile, umetumia mkabala wa kiidadi na wa kitaamuli kuwasilisha na kujadili data. Matokeo ya utafiti huu yameonesha kwamba wanafunzi wa Shule za Msingi wanafundishwa na wanatumia viakifishi vichache. Viakifishi hivyo ni nukta, kiulizo, mkato na mshangao, huku vingine vikitumika mara chache. Pia, matokeo ya utafiti yameonesha kuwa wanafunzi hawawezi kuakifisha kazi zao kwa usahihi kwa sababu hawafundishwi uakifishaji kwa kina, marefu na mapana. Kwa hali hiyo, wanafunzi hao huandika sentensi bebanifu, sentensi tata na vipande sentensi. Kwa hiyo, utafiti huu unapendekeza uakifishaji kufundishwa kama mada inayojitegemea katika viwango vyote vya elimu, Shule za Msingi, Sekondari hadi Vyuo Vikuu, ili wanafunzi waweze kuzielewa sheria na kanuni za uakifishaji na hivyo kuboresha maandiko yao ya kitaaluma.