John, B. N.2024-03-202024-03-202023John, B. N. (2023). Uchunguzi wa tafsiri ya lugha ya ishara katika riwaya teule, (Doctoral Thesis) The University of Dodoma.https://repository.udom.ac.tz/handle/20.500.12661/4339Tasinifu hii inatokana na utafiti kuhusu uchunguzi wa tafsiri ya lugha ya ishara katika riwaya teule. Utafiti uliofanyika uliongozwa na malengo mahususi matatu yafuatayo: Mosi, kubainisha vipengele vya lugha ya ishara iliyotafsiriwa katika riwaya teule. Pili, kufafanua mbinu za kisanaa zilizotumika kutafsiri lugha ya ishara katika riwaya teule. Tatu, kuchambua upungufu wa tafsiri ya lugha ya ishara katika riwaya teule. Aidha, utafiti uliofanyika uliongozwa na nadharia mbili, nazo ni Nadharia ya Semiotiki na Nadharia ya Ulinganifu wa Kimawasiliano. Nadharia hizi zilitumika katika hatua za ukusanyaji wa data, uchanganuzi wa data, na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti. Ukusanyaji wa data ulihusisha njia kuu mbili, uchambuzi wa matini na usaili. Njia ya uchambuzi wa matini ilihusisha usomaji wa riwaya teule ambazo ni Wema Hawajazaliwa na Shetani Msalabani pamoja na matini chanzi zake. Njia ya usaili ilihusisha usaili wa watafitiwa ishirini na mmoja. Matokeo ya utafiti yanadhihirisha kuwa vipengele vya lugha ya ishara iliyotafsiriwa katika riwaya teule inahusisha matumizi ya wahusika na uhusika wa kiishara, matukio ya kiishara, mandhari ya kiishara, jina la riwaya la kiishara na dhana mbalimbali za kiishara. Pia, matokeo yanaonesha mbinu mbalimbali za kisanaa zilizotumika kutafsiri lugha ya ishara katika riwaya teule. Mbinu hizo ni: matumizi ya hadithi, utomeleaji, motifu ya safari, matumizi ya tamathali za semi, na matumizi ya taswira za kiishara. Aidha, imebainika kuwa kuna upungufu wa tafsiri ya lugha ya ishara katika riwaya teule. Upungufu huo unatokana na upotoshaji, udondoshaji, tofauti za kiutamaduni na tofauti za kisarufi matamshi. Utafiti uliofanyika umeleta mchango mpya ufuatao: Mosi, umechunguza tafsiri ya lugha ya ishara kwa umahususi wake na si kuangalia tafsiri ya vipengele vya fasihi kwa ujumla. Pili, umeweka bayana umuhimu wa tafsiri ya lugha ya ishara katika matini za kifasihi. Tatu, umeonesha namna tafsiri ya neno moja moja linavyoweza kuibua lugha ya ishara kupitia matukio na mandhari ya kiishara. Nne, umefanya ukuzaji wa wigo wa kimatumizi wa Nadharia ya Semiotiki na Nadharia ya Ulinganifu wa Kimawasiliano. Kwa ujumla, utafiti uliofanyika unapendekeza tafiti zijazo zijikite katika tanzu nyingine za fasihi andishi kama vile tamthilia na ushairi ambazo nazo hutumia lugha ya ishara.otherUchunguzi wa tafsiri ya lugha ya ishara katika riwaya teuleThesis