Ngatungwa, Felista J.2021-05-042021-05-042020Ngatungwa, F. J. (2020). Usawiri wa falsafa ya Kiafrika katika semi: mifano kutoka vitendawili vya Kiswahili (Tasnifu ya Umahiri). Chuo Kikuu cha Dodoma, Dodoma.http://hdl.handle.net/20.500.12661/2919Tasnifu (Shahada ya Umahiri katika Fasihi ya Kiswahili)Tasnifu hii inayoitwa “Usawiri wa Falsafa ya Kiafrika katika Semi: Mifano kutoka Vitendawili vya Kiswahili” iliongozwa na malengo mahsusi matatu. Nayo ni, mosi, kubainisha vijenzi vya falsafa ya Kiafrika katika muktadha wa kitamaduni. Pili, kujadili falsafa ya Kiafrika kama inavyojitokeza katika vitendawili vya Kiswahili na tatu, kutathmini athari ya falsafa ya Kiafrika kwa jamii kama inavyosawiriwa katika vitendawili vya Kiswahili. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Kisosholojia kupitia misingi yake kama ilivyofafanuliwa katika utafiti huu. Nadharia hii ilitumika katika michakato ya ukusanyaji wa data, uchambuzi na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti. Utafiti huu ni wa kitaamuli, umetumia usanifu wa kifenomenolojia katika ukusanyaji na uchanganuzi wa data. Utafiti huu ulifanywa uwandani na maktabani. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu za mahojiano, mijadala ya vikundi lengwa na udurusu wa nyaraka. Eneo la utafiti lilihusisha mikoa ya Kagera na Dodoma. Sampuli ya utafiti iligawiwa katika makundi matatu. Nayo ni wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari, wanajamii wenye umri kuanzia miaka hamsini na tano na kuendelea na maandiko kuhusu vitendawili vya Kiswahili na falsafa ya Kiafrika. Sampuli ilipatikana kwa kutumia mbinu ya sampuli lengwa ya mpokezo na wa kutegemeafursa. Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa falsafa ya Kiafrika hudhihirika kupitia mambo mbalimbali yanayojitokeza katika maisha ya mwanadamu. Mambo hayo ni suala la umoja na ushirikiano, ndoa na uzazi, “uchawi na ushirikina”, uhai na kifo, uduara, maadili na suala la imani katika Mungu na mizimu. Aidha, kupitia mifano mbalimbali ya vitendawili vya Kiswahili, utafiti umebaini kuwa, utanzu wa vitendawili una hazina kubwa katika kuhifadhi na kutunza maarifa ya falsafa ya Kiafrika na pia falsafa hiyo ina athari kubwa katika maisha ya jamii ya Kiafrika. Utafiti umependekeza kuwa bado kuna haja ya tafiti nyingi zaidi kufanyika katika uga wa fasihi simulizi, ili kubaini ni kwa namna gani tanzu za fasihi hiyo zinaweza kutumika kama darasa la kufunza na kuhifadhi maarifa ya kifalsafa ya jamii za Waafrika.KiswSemiVitendawiliFalsafaKiswahiliKiafrikaKiafrika falsafaVitendawili kiswahiliVijenzi falsafaUsawiri wa falsafa ya Kiafrika katika semi: mifano kutoka vitendawili vya KiswahiliDissertation