Browsing by Author "Faustine, Stella"
Now showing 1 - 3 of 3
Results Per Page
Sort Options
Item Falsafa ya waafrika na ujenzi wa mtindo wa uhalisiajabu katika riwaya ya Kiswahili(Chuo kikuu cha Dodoma, 2017) Faustine, StellaTasnifu hii ni zao la utafiti uliofanywa unaohusu Falsafa ya Waafrika na Mchango Wake katika Ujenzi wa Mtindo wa Uhalisiajabu katika Riwaya ya Kiswahili. Utafiti uliozalisha tasnifu hii umetokana na changamoto kubwa kuwa upo ugumu wa uelewekaji wa maudhui ndani ya kazi za Fasihi zinazotumia mtindo wa uhalisiajabu. Ili kutimiza azma ya kufanyika kwa utafiti huu, malengo manne yalishughulikiwa. Nayo ni kubainisha namna Falsafa ya Waafrika ilivyosawiriwa katika riwaya teule za Kiswahili za kihalisiajabu, kujadili namna Falsafa hiyo inavyojitokeza kama kijenzi cha mtindo wa uhalisiajabu katika riwaya teule za Kiswahili za kihalisiajabu, kuainisha mtindo ya uhalisiajabu kwa kuzingatia namna unavyojitokeza katika riwaya teule za Kiswahili za kihalisiajabu, na kufafanua mchango wa mtindo wa uhalisiajabu katika maendeleo ya riwaya ya Kiswahili. Njia zilizotumika kupata data za utafiti uliozalisha tasnifu hii ni usaili, udodosaji, udurusu wa nyaraka na ushuhudiaji. Data za utafiti huu zilitafsiriwa na kuchambuliwa kwa kutumia nadharia tete ya Uhalisiajabu. Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa kusawiriwa kwa Falsafa ya Waafrika katika riwaya za Kiswahili kuna mchango mkubwa katika kuujenga mtindo wa uhalisiajabu. Aidha, imebainika pia kuwa kuna aina mbalimbali za mtindo wa uhalisiajabu katika riwaya za Kiswahili za kihalisiajabu. Nazo ni: uhalisiajabu fantasia, tarazi, fifi, wa kimajazi, na wa kisitiari. Kwa upande mwingine, matokeo ya utafiti yameonesha kuwa mtindo wa uhalisiajabu una mchango mkubwa katika maendeleo ya riwaya ya Kiswahili, kifasihi na kijamii. Kifasihi, mtindo huu umechangia katika maendeleo ya riwaya ya Kiswahili kiepistemolojia, kiujumi, na katika upanuzi wa uhuru wa waandishi katika kuandika kazi zao. Kijamii, mtindo huu umeifanya riwaya ya Kiswahili kuwa ni darasa la kujifunza maarifa ya Falsafa ya Waafrika; na pia, kama ghala la kuhifadhia amali za Waafrika. Utafiti umehitimishwa kwa kupendekeza mambo makuu mawili yafuatayo: Mosi, Serikali kuweka mikakati mathubuti ya kuhakikisha kuwa lugha na Fasihi ya Kiswahili vinapewa kipaumbele katika muktadha wa elimu na jamii kwa jumla. Pili, Usomaji wa kazi za Fasihi ufanywe kwa umakini kwa kuzingatia nadharia za uhakiki zinazoendana na kazi husika na muktadha wa jamii.Item Msukumo wa jamii katika mabadiliko ya utendaji wa tamthilia ya kiswahili(Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 2020) Faustine, StellaTafiti mbalimbali zimekuwa zikijadili kuhusu tamthilia ya Kiswahili kwa kuangalia historia, maendeleo yake pamoja na vipengele vinavyounda utanzu huo kwa jumla. Vipengele vingine hasa vya mabadiliko ya utendaji wa tamthilia pamoja na msukumo wa kijamii katika kuzua mabadiliko hayo havikupewa kipaumbele. Hali hii imesababisha mabadiliko ya utendaji wa sanaa mbalimbali za maonyesho kama vile tamthilia, kutohusishwa na mabadiliko ya jamii, hivyo kusababisha ugumu katika kuelewa maudhui yaliyomo ndani yake kwa kina. Makala haya yanalenga kuziba pengo hilo kwa kuonesha namna msukumo wa jamii hususan uvumbuzi wa sayansi na teknolojia unavyochangia mabadiliko ya utendaji wa tamthilia. Makala yametumia data za maktabani ambazo zilipatikana kupitia njia ya udurusu wa nyaraka, mapitio ya tamthilia zilizohifadhiwa katika mfumo wa kidijiti, na usomaji makini wa tamthilia andishi. Data zilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa kutumia mkabala wa kitaamuli ambao hutumia maelezo katika uwasilishaji wa maudhui. Aidha, Nadharia ya Uhalisia imetumika katika uchanganuzi wa data na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti. Makala yamebainisha kuwa mabadiliko yaliyotokea katika jamii kama vile maendeleo ya uvumbuzi wa sayansi na teknolojia, yana mchango mkubwa katika mabadiliko ya utendaji wa tamthilia. Kimsingi, makala yanatoa hamasa kwa waandishi na wahakiki wa tamthilia ya Kiswahili katika kuyahusisha maendeleo ya tamthilia na mabadiliko ya jamiiItem Uafrikanishaji katika riwaya ya kiswahili(Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 2020) Faustine, StellaMakala haya yanajadili namna uchimuzi wa falsafa ya Waafrika unavyochangia kuipa fasihi ya Kiswahili sura ya Uafrika. Vipengele vilivyojadiliwa katika makala hii ni uzazi na ulezi kama jambo la muhimu kwa Waafrika, imani kuhusu uchawi, kuwapo kwa ulimwengu wenye matabaka matatu, mwendelezo wa maisha baada ya kifo na mtazamo kuhusu kuwapo kwa busara na hekima kwa wazee. Swali linaloibuliwa na kujibiwa na makala haya ni kuwa, je, ni kwa namna gani falsafa ya Waafrika imesawiriwa katika fasihi ya Kiswahili, na hivyo, kuifanya kuwa na sura ya Uafrika? Makala yanajibu swali hili kwa mifano hai kutoka katika riwaya za Kiswahili zilizoandikwa kwa kufuata mkondo wa kimajaribio ambazo ni Nagona (1990) ya E. Kezilahabi, Babu Alipofufuka (2001) ya S. AMohammed na Bina – Adamu! (2002) ya K. W. Wamitila.