Browsing by Author "Hakimu, Johari"
Now showing 1 - 1 of 1
Results Per Page
Sort Options
Item Ubantuishaji wa kimofolojia katika vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu(Chuo Kikuu cha Dodoma, 2020) Hakimu, JohariPamoja na kwamba lugha ya Kiswahili ina maneno mengi yaliyokopwa katika lugha ya Kiarabu, haijawa wazi ni kwa namna gani maneno hayo (hasa vitenzi) ya Kiswahili yenye asili ya Kiarabu yamepata sifa za Kibantu. Kwa hiyo, kuna masuala kadhaa kuhusu ubantuishaji wa vitenzi vya mkopo ambayo hayajawa wazi. Masuala hayo ni kama vile ubainishaji wa maumbo ya vitenzi, ufafanuzi wa michakato ya kimofolojia inayopitiwa katika ubantuishaji wa vitenzi hivyo, na tathmini ya mwelekeo wa ubantuishaji wa vitenzi hivyo. Utafiti ulifanyika katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo ulihusisha maeneo ya Tanzania bara na Zanzibar. Data ya utafiti huu ilikusanywa kwa njia tatu ambazo ni: upitiaji wa nyaraka, usaili na upimaji wa usahihi wa kisarufi. Katika uchanganuzi na ufasiri wa data, Nadharia ya Mofolojia Leksika na Nadharia ya Usarufishaji zilitumika. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa, msambao wa vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu katika ruwaza ya vitenzi vya Kibantu unachukua maumbo kumi (10) kati ya kumi na moja (11) ya ruwaza hiyo sawa na vitenzi vya Kiswahili asilia. Tofauti kubwa ya vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu imebainika katika baadhi ya michakato ya ubantuishaji ya vitenzi hivyo. Vilevile, viambishi vya vitenzi vimechanganuliwa katika darajia nne zenye kuakisi michakato ya unyambuzi au uambatizi wa viambishi husika. Darajia hizi pia zinaakisi viwango vya ukale wa viambishi vya Kiswahili. Ukale huo umepimwa kwa enzi za kabla ya Kiswahili kukutana na Kiarabu. Baadhi ya viambishi visivyojitokeza katika vitenzi vyenye asili ya Kiarabu ni vyenye ukale wa zamani zaidi, na kwamba michakato yake kimofolojia na kifonolojia ilishakoma kabla Kiarabu kukutana na Kiswahili. Pia, vitenzi vilivyochanganuliwa kimofolojia, mwelekeo wake wa ubantuishaji umebainika kwa kutumia Nadharia ya Usarufishaji. Kutokana na nadharia hiyo, ukamilifu na usiukamilifu wa ubantuinshaji wa vitenzi hivyo umebainishwa. Ukamilifu na usiukamilifu umebainika kutokana na matumizi ya ruwaza ya vitenzi vya Kibantu na michakato ya ubantuishaji. Kwa kuwa utafiti huu umechunguza vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu, tafiti zijazo zinaweza kuchunguza aina nyingine za maneno. Hata hivyo, kwa kuwa usarufishaji hufanyika taratibu halikutolewa hitimisho la kuonesha ubantuishaji wa vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu unapokomea.