Browsing by Author "Masimo, D. B."
Now showing 1 - 1 of 1
Results Per Page
Sort Options
Item Mkengeuko wa utamaduni wa waswahili katika riwaya ya kiswahili zama za utandawazi: mifano kutoka riwaya teule(The University of Dodoma, 2023) Masimo, D. B.Tasnifu hii ni matokeo ya utafiti uliofanywa kuhusu “Mkengeuko wa Utamaduni wa Waswahili katika Riwaya ya Kiswahili Zama za Utandawazi”. Riwaya zilizochunguzwa ni miongoni mwa zilizoandikwa katika zama za utandawazi ambazo ni: Rais Anampenda Mke Wangu na Almasi za Bandia. Pia, utafiti ulichunguza riwaya zilizoandikwa kabla ya utandawazi ili kupata picha ya jinsi utamaduni wa Waswahili ulivyokuwa kwa wakati huo. Riwaya hizo ni: Mirathi ya Hatari na Kurwa na Doto. Utafiti huu ulichunguza namna mkengeuko wa utamaduni wa Waswahili unavyojitokeza katika riwaya teule za Kiswahili tofauti na vyanzo vingine kama redio, televisheni na mitandao ya kijamii kwa kuwa riwaya hizo zimesawiri kwa uhalisia mkengeuko wa utamaduni wa Waswahili. Utafiti uliongozwa na malengo mahususi matatu: Mosi, kubainisha vipengele vya utamaduni wa Waswahili katika riwaya teule za Kiswahili kabla ya utandawazi. Pili, kufafanua namna mkengeuko wa utamaduni wa Waswahili unavyojitokeza katika riwaya teule za zama za utandawazi. Tatu, kutathimini athari za mkengeuko wa utamaduni wa Waswahili katika riwaya ya Kiswahili zama za utandawazi. Utafiti uliongozwa na nadharia mbili: Nadharia ya Sosholojia na nadharia ya UbaadaUkoloni. Nadharia ya Sosholojia ilitumika kuchunguza vipengele vya utamaduni wa Waswahili vilivyopo katika riwaya teule. Pia, nadharia ya Ubaada Ukoloni ilitumika katika kuangalia mabadiliko yaliyochangiwa na taathira za ukoloni katika nchi zilizotawaliwa na wakoloni. Njia zilizotumika kukusanya data ni usaili na uchanganuzi matini. Njia ya usaili ilitumia sampuli ya wanafunzi na wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma kulingana na mwongozo wa maswali ya utafiti huu. Pia, uchanganuzi wa matini ulipitia riwaya teule za Kiswahili ambazo zilichanganuliwa kulingana na malengo ya utafiti. Utafiti ulifanyikia katika mkoa wa Dodoma. Data zilikusanywa katika Chuo Kikuu cha Dodoma katika Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii. Matokeo ya utafiti yamebaini kuwapo kwa mkengeuko wa utamaduni wa Waswahili katika vipengele vya lugha, ndoa, imani za kidini, kifo, maadili na mavazi. Utafiti huu umetoa mchango mpya kwa jamii kwa kuonyesha namna riwaya ya Kiswahili inavyokuwa wakala mmojawapo wa kukengeusha utamaduni wa Waswahili katika zama za utandawazi mbali na vyanzo vingine kama filamu, mitandao ya kijamii, redio na televisheni ambavyo vinachangia kumomonyoa maadili katika jamii.