Doctoral Theses
Permanent URI for this collection
Browse
Browsing Doctoral Theses by Author "Ponera, Athumani Salum"
Now showing 1 - 1 of 1
Results Per Page
Sort Options
Item Ufutuhi katika nathari ya Kiswahili ulinganisho wa nathari za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi(Chuo kikuu cha Dodoma, 2014) Ponera, Athumani SalumTasnifu hii inajadili jinsi ufutuhi unavyotumiwa katika nathari ya Kiswahili. Hoja kuu ya tasnifu ni kwamba nathari za waandishi teule, Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi, zimeundwa kwa kutumia ufutuhi kama mbinu mojawapo ya kibunilizi inayotumiwa pia na Watanzania katika maisha yao ya kila siku. Dhana ya ufutuhi imetafitiwa na kuelezwa kama dhana jumuifu inayomaanisha kwa pamoja kicheko, tabasamu, raha, na furaha ambayo huweza kuletwa na maneno au matendo au mazingira yoyote kupitia vijenzi kama vile vijembe, dhihaka, kejeli, tashtiti, ufyosi, na utani. Kimsingi, kichokozi kikubwa cha kufanyika kwa utafiti ulioizaa tasnifu hii ni utafiti mwingine uliofanywa na Ponera (2008 - 2010) ambao ulichunguza jinsi Shaaban Robert alivyoitumia mbinu ya ufutuhi katika riwaya zake. Utafiti huu mpya ulipanua utafiti tangulizi kwa: kulinganisha ufutuhi uliomo katika bunilizi za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi, kuchunguza jinsi mbinu hii ya ufutuhi inavyotokea na kutumiwa na Watanzania, kulinganisha na kulinganua miktadha iliyowasababisha waandishi teule watumie mbinu hii katika nathari zao, pamoja na kulinganisha na kulinganua utokeaji na mtawanyo wa matukio ya kifutuhi katika makundi yote matatu ya nathari za waandishi teule. Kwa hiyo, katika kufanya mjadala, sehemu ya data zilizoijenga tasnifu hiyo ya 2010 zimerejelewa na kupanuliwa. Utafiti ulifanyika maktabani na uwandani kupitia mbinu za udurusu wa maandiko, usaili, mjadala wa vikundi, na ushuhudiaji. Utafiti na uchambuzi wa data uliongozwa na misingi ya nadharia za Upokezi na Ukanivali. Upokezi ulitumika zaidi kutathminia maoni ya watafitiwa kuhusu kuwapo au kutokuwapo kwa mwelekeo wa kifutuhi katika nathari za waandishi teule. Ukanivali ulihusika zaidi na ubainishaji na uchambuzi wa matukio yenyewe ya kifutuhi. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa katika maisha ya Watanzania ufutuhi hujitokeza kama tukio la kifasihi, tukio la kijamii, tukio la kiujumi, au kama kiambata cha msingi katika maisha ya sasa. Aina za ufutuhi zilizobainika katika nathari za waandishi teule ni tano. Aina hizo ni ufutuhi wa utwezaji ambao msingi wake ni matumizi ya ufyosi au matusi, ufutuhi wa balagha unaoegemea katika utiaji chumvi, na ufutuhi wa unyume ambao msingi wake ni uwasilishaji wa jambo kwa hali ya upindu kupitia kejeli, dhihaka, vijembe, tashtiti, na utani. Nyingine ni ufutuhi wa majazi unaoegemea katika matumizi ya lakabu, pamoja na ufutuhi wa utanakuzi unaojengwa na mnato na mvuto unaotokana na uteuzi na mpangilio wa maneno. Tofauti za ufutuhi uliomo katika bunilizi za waandishi hawa zinatokana na: silika na tajiriba zao, utamaduni, mikabala ya kiitikadi na kifalsafa, pamoja na masafa ya kiwakati. Ufutuhi uliotumiwa katika nathari hizo huipatia hadhira tija za kijamii, za kipedagojia, za kiafya, za kiujumi, pamoja na za kiepistemolojia. Kwa upande wa madhara, mbinu hii huweza kuleta madhara ya kimaadili kwa hadhira, yale ya kiutunzi kwa mtunzi mwenyewe, pamoja na madhara ya kijamii. Upo mchango mpya ulioibuliwa na utafiti huu katika taaluma ya fasihi; nao ni huu ufuatao: Mosi, ufafanuzi wa dhana yenyewe ya ufutuhi kama dhana jumuifu. Pili, kufafanuliwa kwa nadharia tatu za ufutuhi (Mkwezo, Msigano na Burudiko) zinazoelezea jinsi ufutuhi unavyoweza kutokea (kupitia ama ridhiko la nafsi au kuwapo kwa pengo au msigano baina ya uwasilishaji na uhalisi wake). Tatu, ni kubainishwa kwa misingi ya taaluma ya Fasihi Linganishi inayoweza kutumika katika tafiti zenye mwelekeo wa kiulinganishaji. Nne, kuibuliwa kwa aina tano za ufutuhi zilizodokezwa katika aya ya hapo juu. Tano, kuibuliwa kwa tija na madhara ya mbinu hii. Na, sita, ni kuitambulisha dhana ya ufutuhi kama umbo la kitaaluma.