Browsing by Author "Kasiga, Gerevaz. A."
Now showing 1 - 5 of 5
Results Per Page
Sort Options
Item Dhima ya sadfa ya kimapenzi katika kujenga matukio ya ‘kishushushu’ na ‘kijasusi’: uchunguzi wa riwaya ya kikosi cha kisasi(The University of Dar es Salaam, 2022) Kasiga, Gerevaz. A.; Maffa, Eliamini MShabaha ya makala haya ni kufafanua matumizi ya sadfa ya kimapenzi katika kuwasaidia watunzi kujenga tungo mbalimbali za kisanaa na kutimiza au kukamilisha uwasilishaji wa matukio ya kishushushu na kijasusi. Ufafanuzi wetu umemakinikia riwaya ya Kikosi cha Kisasi ya mwandishi Aristablus Elvis Musiba. Sadfa ni hali ya utokeaji wa matukio kwa wakati mmoja kwa namna inayoshangaza au inayoashiria bahati. Hii ni miongoni mwa mbinu zinazotumiwa na watunzi katika kuzijenga na kuzikamilisha tungo zao (Wamitila, 2003; Dannenberg, 2008). Mara nyingi watunzi wa kazi za kifasihi huitumia mbinu hii sambamba na mbinu nyingine katika kufanikisha azma ya tungo hizo. Mbinu hizo nyingine zaweza kuhusisha uhalisiajabu, utanzia, ufutuhi, na usemezano. Kazi ya kifahisi hujengwa kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisanaa zinazoafikiana na lengo pamoja na aina ya kazi ya kifasihi inayowasilishwa. Sadfa ni mojawapo ya mbinu hizo za kisanaa ambayo hutumiwa na watunzi kuibua, kujenga na kukamilisha azma ya tungo zao. Katika mjadala wa makala haya tumeonesha namna sadfa ya kimapenzi ilivyotumika kwenye miktadha ya kutiana moyo wa kufanikisha kazi ya kishushushu na kijasusi; kuleta urahisi wa ufanikishwaji wa kazi ya kishushushu na kijasusi; kusaidia uokozi na uchocheaji kisasi; na mwishowe kusababisha uvumbuzi wa taarifa muhimu za kijasusi pamoja na ukamilishwaji wa operesheni za kijasusi. Katika riwaya teule mwandishi ameitumia mbinu hii kupitia mahusiano ya kimapenzi baina ya mhusika wake mkuu Willy Gamba (mwanamume) pamoja na wahusika wasaidizi (mabinti) Amanda, Ntumba, Mwadi na Tete.Item Filamu ya Kiswahili: Fasihi simulizi iliyostawi(Moi University Press, 2019) Kasiga, Gerevaz. A.; Luhwago, Neema. J.Makala haya yanaijadili sanaa ya filamu za Kiswahili kama fasihi simulizi iliyopevuka na kuchukua mkondo wa kiteknnlojia kutokana na utegemezi wake wa nyenze katika utambaji. Hadhi ya kisanaa ya filamu imetazamwa kwa namna inayoonesha kujitokezea kwake kupitia umbo na wajihi wa kifasihi.Item Mdhihiriko wa kionjo cha usangwini kwa mhusika Willy Gamba katika riwaya ya Njama(The University of Dar es Salaam, 2020) Ponera, Athumani S.; Kasiga, Gerevaz. A.Maudhui ya kazi za kifasihi hufika kwa hadhira kupitia wahusika. Watunzi huwajenga wahusika hao kwa kutumia mbinu mbalimbali huku wakiwavisha haiba na mujukumu ambayo, aghalabu, huendana na vionjo maalumu vya haiba (psychological temperaments). Shabaha ya makala hii ni kufafanua namna ambavyo sifa na majukumu ya mhusika wa kazi za kifasihi huendana na vionjo vya kihaiba anavyojengwa navyo. Ufafanuzi wetu unaegemezwa kwenye uhusika wa Willy Gamba katika riwaya ya Njama. Tunaonesha namna anavyotekeleza majukumu yake kwa kuongozwa na sifa za kionjo cha usangwini ambacho ni mojawapo ya vionjo vikuu vinne vya kihaiba.Item Miktadha ya matumiziya U-Nigeria katika video za nyimbo za muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania(University of Dodoma, Tanzania, 2022) Kasiga, Gerevaz. A.Tasnia ya Muziki wa Kizazi Kipya wa Kiswahili nchini Tanzania imetekwa na utamaduni wa nje, hususani wa Kinigeria. Hali hii ikiendelea itapoteza utambulisho wa Kitanzania katika sanaa. Kwa hali hiyo, makala imechunguza miktadha ya matumizi ya U-Nigeria katika video za nyimbo za muziki wa kizazi kipya wa Kiswahili nchini Tanzania ili kubaini misukumo yake na kutazama njia za kuupunguza na kuuondosha. Makala imetumia mkabala wa kitaamuli. Data zilikusanywa maktabani na uwandani. Nadharia ya Uhalisia ilitumika kama kiunzi cha uchambuzi na mjadala. Hatimaye, makala imebaini miktadha saba ya utumiwaji wa U-Nigeria. Miktadha hiyo imehusisha mivuto ya kiubidhaishaji, matumizi ya vyombo vya habari, mivuto ya kiujumi na kibunifu, na mivuto kutokana na mwigo kutoka wasanii nguli. Miktadha mingine imehusisha misukumo ya wasikilizaji na watazamaji, ukosefu wa alama ya utambulisho wa kitamaduni, na ukosefu wa elimu ya tasnia ya muziki. Mwisho, imependekezwa kuwa ili kulinda utamaduni wa Kitanzania kupitia muziki, ni vema wasanii wapatiwe warsha, semina, na madarasa maalumu ya kukuza vipaji vyao kwamaslahi ya jamii nzima ya Watanzania.Item Uibukaji wa U-nigeria katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania: masuala muhimu ya kuzingatia(Utafiti Foundation, 2023) Kasiga, Gerevaz. A.Imebainika kuwa tasnia ya muziki wa kizazi kipya wa Kiswahili nchini Tanzania imetekwa na utamaduni wa nje hususani wa Kinigeria (Mrikaria, 2007; Kasiga, 2022). Athari zake zimebainika katika vipengele kadhaa vya kibunifu (Kasiga, 2021). Pia, misukumo mbalimbali inayowasukuma wasanii kutumia U-Nigeria imebainishwa (Kasiga, 2022). Kimsingi, hali hii inatishia utambulisho wa Kitanzania katika sanaa. Hivyo, makala hii imetoa mapendekezo ya kiuboreshaji dhidi ya UNigeria katika video za nyimbo za muziki wa kizazi kipya wa Kiswahili nchini Tanzania. Mapendekezo yaliyotolewa yamehusisha: kufanyika uwekezaji wa muziki wa asili wa Kitanzania, kufanyika kwa usimamizi maalumu katika vyombo vya habari, kuwepo kwa sheria na kanuni za kulinda uasili wa muziki wa kizazi kipya, na uanzishwaji wa semina, warsha pamoja na madarasa maalumu kwa wasanii. Isitoshe, makala imependekeza kuwepo kwa agenda mahususi ya kitaifa kujenga uzalendo, kumakinikia mitindo ya sanaa za Kitanzania katika utengenezaji wa muziki, kuharakisha upatikanaji wa vazi la taifa, kuanzishwa kwa vipindi vya uchambuzi wa nyimbo, na wasanii kushawishiwa kutumia mandhari ya Kitanzania katika video zao. Zaidi, imependekezwa kuanzishwa kwa matamasha na tuzo za muziki, asasi za elimu kutengeneza mitaala ya biashara, lugha ya Kiswahili, na utamaduni wa Kitanzania, na kuwe na muumano kati ya biashara, utamaduni na teknolojia.