Doctoral Theses
Permanent URI for this collection
Browse
Browsing Doctoral Theses by Subject "Euphrase Kezilahabi"
Now showing 1 - 2 of 2
Results Per Page
Sort Options
Item Falsafa ya riwaya za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi katika muktadha wa epistemolojia ya Kibantu(The University of Dodoma, 2016) Chuachua, RashidTasnifu hii inayoitwa ―Falsafa ya Riwaya za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi katika Muktadha wa Epistemolojia ya Kibantu‖ imechunguza namna maarifa ya Wabantu yanavyojitokeza katika riwaya za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi. Uchunguzi huo umezingatia vipengele mbalimbali kama vile uchawi, tambiko, imani au fikra zao kuhusu roho na kifo, moyo, Mungu, mwanya, uzazi, utoaji majina, uganga na ardhi. Taarifa zilikusanywa kwa njia ya mahojiano, majadiliano katika vikundi, mapitio ya maandiko na ushuhudiaji. Taratibu za ukusanyaji wa data ziliongozwa na mkabala wa kifinomenolojia, wakati uchanganuzi wa taarifa uliongozwa na mkabala wa kiepistemolojia. Finomenolojia ni mkabala maarufu katika utafiti wa kitaamuli; epistemolojia ni mkabala mpya katika uchambuzi wa kazi za fasihi. Matumizi ya mkabala huu yamedhihirisha kuwa Wabantu wana namna yao ya kupata maarifa ambayo ni kupitia kani-uhai toka kwa Mungu wao. Wazee walio hai ndiyo chanzo cha maarifa hapa duniani kwa kuwa wana uwezo wa kuwasiliana na wahenga wao kwa urahisi zaidi. Aidha, kujua kwao kumefungwa kwenye duara linalofanywa na kani-uhai toka kwa Mungu, kuja kwa wahenga, kisha kwa watu walio hai na kurudi tena kwa Mungu. Mungu ndiye chanzo kikuu cha kani-uhai. Aliye nje ya duara hili linaloundwa na kani-uhai, hawezi kuwa na maarifa ya kaida za jamii yake. Kwa Wabantu, maarifa ni kujua asili ya kani-uhai na athari zake. Jambo hili hutokana na uzoefu wa muda mrefu wa kaida za jamii husika; pamoja na kudumisha mila na desturi zinazoimarisha uhusiano uliopo ndani ya duara la maisha. Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa; pamoja na kuyaweka mawazo ya Falsafa za Ulaya na Asia katika maandishi yao, kwa kiasi kikubwa, kazi za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi zinawasilisha maarifa halisi ya Wabantu. Utafiti umebaini kuwa maarifa ya Wabantu yanaegemea katika misingi ya kiontolojia. Hivyo basi, ontolojia ndiyo kiini cha epistemolojia ya Kibantu. Katika kudhihirisha hili, vigezo vinavyotumiwa na Wabantu katika kumbainisha mtu vimewekwa bayana. Utafiti pia umebaini kuwa waandishi hawa wawili hawakumwacha mtu akiwa hewani, bali baada ya kumbainisha kwa mujibu wa maarifa yao, wamemweka katika jamii na kumwonyesha anavyothamini amali za jamii yake. Amali hizo ni za kidini au kiimani, kimaarifa na kimatendo. Aidha, utafiti umebaini kuwa uandishi wao umejiegemeza katika mikondo ya Falsafa ya Kiafrika ya kiethinofilosofia na kihekima kama ilivyoasisiwa na Placid Tempels na Odera Oruka kwa kufuatana. Kwa jumla, maarifa au epistemolojia ya Kibantu yameonekana yakiegemea ontolojia kwa kila kipengele; na hivyo, kani-uhai kuonekana kama mhimili mkuu wa falsafa ya Kibantu. Utafiti ulioizaa tasnifu hii umeonekana kuwa na mchango mkubwa katika eneo la Falsafa ya Kiafrika na ya Kibantu. Kwa maoni na upeo wa mtafiti, yumkini, hii ni Tasnifu ya kwanza nchini Tanzania ya kiwango cha shahada ya uzamivu, iliyochokoza taaluma ya Fasihi kwa mtazamo wa falsafa ya Kibantu kwa kutumia riwaya za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi. Vilevile, ni ya kwanza kuutumia mkabala wa epistemolojia ya Kibantu katika uchanganuzi wa kazi za Fasihi. Nadharia hii mpya iliyoegemea uchambuzi wa fikra za Wabantu inaweza kutumiwa na watafiti wengine. Hali hii itasaidia kutotumia nadharia za kigeni pekee katika kuchunguza fasihi ya Kiswahili, hata kwa mambo yasiyohusiana na mitazamo ya kigeni.Item Ufutuhi katika nathari ya Kiswahili ulinganisho wa nathari za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi(Chuo kikuu cha Dodoma, 2014) Ponera, Athumani SalumTasnifu hii inajadili jinsi ufutuhi unavyotumiwa katika nathari ya Kiswahili. Hoja kuu ya tasnifu ni kwamba nathari za waandishi teule, Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi, zimeundwa kwa kutumia ufutuhi kama mbinu mojawapo ya kibunilizi inayotumiwa pia na Watanzania katika maisha yao ya kila siku. Dhana ya ufutuhi imetafitiwa na kuelezwa kama dhana jumuifu inayomaanisha kwa pamoja kicheko, tabasamu, raha, na furaha ambayo huweza kuletwa na maneno au matendo au mazingira yoyote kupitia vijenzi kama vile vijembe, dhihaka, kejeli, tashtiti, ufyosi, na utani. Kimsingi, kichokozi kikubwa cha kufanyika kwa utafiti ulioizaa tasnifu hii ni utafiti mwingine uliofanywa na Ponera (2008 - 2010) ambao ulichunguza jinsi Shaaban Robert alivyoitumia mbinu ya ufutuhi katika riwaya zake. Utafiti huu mpya ulipanua utafiti tangulizi kwa: kulinganisha ufutuhi uliomo katika bunilizi za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi, kuchunguza jinsi mbinu hii ya ufutuhi inavyotokea na kutumiwa na Watanzania, kulinganisha na kulinganua miktadha iliyowasababisha waandishi teule watumie mbinu hii katika nathari zao, pamoja na kulinganisha na kulinganua utokeaji na mtawanyo wa matukio ya kifutuhi katika makundi yote matatu ya nathari za waandishi teule. Kwa hiyo, katika kufanya mjadala, sehemu ya data zilizoijenga tasnifu hiyo ya 2010 zimerejelewa na kupanuliwa. Utafiti ulifanyika maktabani na uwandani kupitia mbinu za udurusu wa maandiko, usaili, mjadala wa vikundi, na ushuhudiaji. Utafiti na uchambuzi wa data uliongozwa na misingi ya nadharia za Upokezi na Ukanivali. Upokezi ulitumika zaidi kutathminia maoni ya watafitiwa kuhusu kuwapo au kutokuwapo kwa mwelekeo wa kifutuhi katika nathari za waandishi teule. Ukanivali ulihusika zaidi na ubainishaji na uchambuzi wa matukio yenyewe ya kifutuhi. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa katika maisha ya Watanzania ufutuhi hujitokeza kama tukio la kifasihi, tukio la kijamii, tukio la kiujumi, au kama kiambata cha msingi katika maisha ya sasa. Aina za ufutuhi zilizobainika katika nathari za waandishi teule ni tano. Aina hizo ni ufutuhi wa utwezaji ambao msingi wake ni matumizi ya ufyosi au matusi, ufutuhi wa balagha unaoegemea katika utiaji chumvi, na ufutuhi wa unyume ambao msingi wake ni uwasilishaji wa jambo kwa hali ya upindu kupitia kejeli, dhihaka, vijembe, tashtiti, na utani. Nyingine ni ufutuhi wa majazi unaoegemea katika matumizi ya lakabu, pamoja na ufutuhi wa utanakuzi unaojengwa na mnato na mvuto unaotokana na uteuzi na mpangilio wa maneno. Tofauti za ufutuhi uliomo katika bunilizi za waandishi hawa zinatokana na: silika na tajiriba zao, utamaduni, mikabala ya kiitikadi na kifalsafa, pamoja na masafa ya kiwakati. Ufutuhi uliotumiwa katika nathari hizo huipatia hadhira tija za kijamii, za kipedagojia, za kiafya, za kiujumi, pamoja na za kiepistemolojia. Kwa upande wa madhara, mbinu hii huweza kuleta madhara ya kimaadili kwa hadhira, yale ya kiutunzi kwa mtunzi mwenyewe, pamoja na madhara ya kijamii. Upo mchango mpya ulioibuliwa na utafiti huu katika taaluma ya fasihi; nao ni huu ufuatao: Mosi, ufafanuzi wa dhana yenyewe ya ufutuhi kama dhana jumuifu. Pili, kufafanuliwa kwa nadharia tatu za ufutuhi (Mkwezo, Msigano na Burudiko) zinazoelezea jinsi ufutuhi unavyoweza kutokea (kupitia ama ridhiko la nafsi au kuwapo kwa pengo au msigano baina ya uwasilishaji na uhalisi wake). Tatu, ni kubainishwa kwa misingi ya taaluma ya Fasihi Linganishi inayoweza kutumika katika tafiti zenye mwelekeo wa kiulinganishaji. Nne, kuibuliwa kwa aina tano za ufutuhi zilizodokezwa katika aya ya hapo juu. Tano, kuibuliwa kwa tija na madhara ya mbinu hii. Na, sita, ni kuitambulisha dhana ya ufutuhi kama umbo la kitaaluma.