Uhusiano wa silika na utendaji wa wahusika wa fasihi ya watoto ya kiswahili: uchunguzi kifani wa ngoma ya mianzi na safari ya prospa
Loading...
Date
2023
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
The University of Dodoma
Abstract
Tasinifu hii ni zao la utafiti uliofanyika kuhusu uhusiano wa silika na utendaji wa wahusika wa Fasihi ya watoto ya Kiswahili. Utafiti uliofanyika uliongozwa na malengo mahususi matatu: Kufafanua namna mbalimbali za utendaji wa wahusika wakuu wa riwaya teule za Fasihi ya watoto, kuchambua aina za silika za wahusika wakuu wa riwaya teule za Fasihi ya watoto, na kutathimini athari za uhusiano baina ya utendaji wa wahusika wakuu wa Fasihi ya watoto na sifa za silika zao. Ili kufikia malengo hayo, uchunguzi kifani wa riwaya za Ngoma ya Mianzi na Safari ya Prospa ulizingatiwa. Utafiti ulifanyika katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam. Tasinifu hii imetumia mkabala wa kitaamuli kwa sababu utafiti ulijikita zaidi katika kuchunguza tabia, hisia, na uzoefu wa wahusika. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu za usaili, usomaji matini, na majadiliano ya vikundi lengwa. Nadharia ya Saikochanganuzi ilisaidia kufikia malengo haya. Nadharia hii imebainisha nafsi na misingi mbalimbali ambayo ilitusaidia katika mchakato mzima wa utafiti uliofanyika. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa wahusika hutenda mambo mbalimbali ili kushauri, kutoa taarifa, kuonya, kudanganya, kushawishi, na kudadisi. Pia, kila mhusika ana silika yake ambayo humtofautisha na mhusika mwingine. Prospa amebainika kuwa na silika ya melankoli na Sara ana silika ya sangwini. Kwa upande mwingine, Mbumi amebainika kuwa na silika ya koleriki na Chulu ana silika ya melankoli. Silika za wahusika zimewasaidia kufikia malengo yao, kwa sababu zimeepusha msuguano kati yao. Vilevile, utafiti ulibaini kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya utendaji na sifa za aina za silika, kwani, ili kutambua silika ya mhusika, ni lazima kuona matendo yake. Pia, silika ndiyo inayomsukuma mhusika kutenda kila akitendacho. Hivyo, tasinifu hii ina umuhimu mkubwa katika uga wa Fasihi ya watoto ya Kiswahili kwa kuwa inaleta chachu kwa watunzi na watafiti kutunga kazi zao kwa kuzingatia aina za silika na kuangalia uhusiano uliopo baina ya Fasihi na saikolojia. Mwisho, tasinifu inatoa mapendekezo kwa serikali, watunzi wa kazi za Fasihi na watafiti. Inapendekeza kuwa serikali ihakikishe inasisitiza usomaji wa vitabu vya ziada ili kukuza usomaji wa kifasihi na kuwawezesha wanafunzi kutambua silika zao kupitia wahusika watakaowasoma. Waandishi, wahakiki, na wataalamu wa Fasihi wafanye ufaraguzi wa kazi hizi ili ziweze kuigizika jukwaani. Hii ni kwa sababu, mambo yote yanayohitajika kwa ajili ya kuigiza yapo katika kazi hizi, kama vile maleba, mandhari, wahusika, na uhusika wao. Kwa hiyo, kupitia uigizaji, watazamaji, hususani watoto watatambua silika zao na za watu wengine wanaowazunguka. Hali hii itasaidia kupunguza migongano na migogoro kwa watoto na jamii kwa jumla.
Description
Keywords
Citation
Mkomwa, S. S. (2023). Uhusiano wa silika na utendaji wa wahusika wa fasihi ya watoto ya Kiswahili: uchunguzi kifani wa ngoma ya mianzi na safari ya prospa, (Doctoal Thesis) The University of Dodoma.