Matumizi ya wakaa katika usimulizi wa riwaya za Kiswahili: Mifano kutoka Nagona na Mzingile

Loading...
Thumbnail Image
Date
2020
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Chuo Kikuu cha Dodoma
Abstract
Tasnifu hii inahusu wakaa katika usimulizi wa riwaya teule za Kiswahili za Nagona na Mzingile zilizotungwa na Euphrase Kezilahabi. Wakaa ni kipengele cha kifani ambacho watunzi wa kazi za kifasihi hukitumia katika kusana kazi zao. Dhana ya wakaa tumeitumia tukimaanisha muda ambao hutumika kutendeka kwa tukio fulani. Dhana hii katika riwaya ya Kiswahili haijachunguzwa vya kutosha; yumkini, hali hii inasababisha kutojulikana miongoni mwa hadhira ya kazi za fasihi. Utafiti ulifanyika maktabani na uwandani (katika miji ya Dodoma na Dar es Salaam). Mbinu ya ufafanuzi ndiyo imetumika kutolea matokeo ya utafiti huu. Nadharia ya naratolojia ilitumika kutokana na mihimili yake kufaa katika kubainisha ruwaza za wakaa, kuchambua misingi iliyomuongoza mtunzi kujenga wakaa katika riwaya teule na kutathmini nafasi ya wakaa katika uelewekaji wa riwaya teule. Tumepata matokeo kwa malengo yote matatu ya utafiti. Katika lengo la kwanza, utafiti umebaini kuwa, wakaa ni mbinu ya kifani inayojitokeza katika kazi za fasihi kwa kutaja ruwaza zake kama vile saa, dakika, mwaka na karne kwa lengo la kwanza. Katika lengo la pili, utafiti umebaini kuwapo kwa misingi ya wakaa kielimu, kijiografia na kiutamaduni. Kielimu, tuna misingi kama ubunifu, utangamano na watunzi wengine, falsafa na upokezi wa hadhira. Kijiografia, kuna msingi wa mazingira. Kiutamaduni, kuna misingi ya dini, mila na desturi. Kuhusu lengo la tatu, utafiti umebaini nafasi ya wakaa katika riwaya kwa jicho la kifani na kwa jicho la kimaudhui. Kifani, tumeangalia udhanaishi na kupeleka matukio mbele. Kimaudhui, tumeeleza namna wakaa unavyotafakarisha wasomaji, kutambulisha wazo rasmi na kubaini uhalisi wa kazi. Mchango mpya ulioibuliwa na tasnifu hii ni kubainisha ruwaza za wakaa kwa wasomaji pamoja na fikra zake. Utafiti umependekeza tafiti zaidi zifanyike juu ya falsafa ya wakaa katika ushairi na tamthiliya pamoja na tanzu za fasihi nenwa.
Description
Tasnifu (MA Kiswahili)
Keywords
Wakaa, Kiswahili, Dodoma, Nagona riwaya, Mzingile riwaya, Riwaya, Riwaya teule, Euphrase Kezilahabi, Fani, Fasihi
Citation
Kinga, J. A. (2020). Matumizi ya wakaa katika usimulizi wa riwaya za Kiswahili: Mifano kutoka Nagona na Mzingile (Tasnifu). Chuo Kikuu cha Dodoma, Dodoma.