Athari za fonolojia ya lugha ya kwanza katika mawasiliano ya wajifunzaji wa kiswahili sanifu kama lugha ya pili: uchunguzi kifani kihehe

Loading...
Thumbnail Image
Date
2023
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
The University of Dodoma
Abstract
Utafiti huu ulihusu athari za fonolojia ya lugha ya Kihehe katika mawasiliano ya wajifunzaji wa Kiswahili Sanifu kama lugha ya pili. Tatizo lililochochea utafiti huu ni upotoshwaji na uharibifu wa maana za maneno unaosababisha kutatizika kwa mawasiliano miongoni mwa wajifunzaji lugha ya Kiswahili Sanifu wa jamii ya Wahehe. Utafiti huu uliongozwa na malengo mahususi manne ambayo ni: kubainisha vipengele vya fonolojia ya Kihehe vinavyohawilishwa katika mawasiliano ya wajifunzaji wa Kiswahili Sanifu kama lugha ya pili; kuchambua athari za fonolojia ya Kihehe katika mawasiliano ya wajifunzaji wa Kiswahili Sanifu kama lugha ya pili; kufafanua sababu za utokeaji wa athari za fonolojia ya Kihehe katika mawasiliano ya wajifunzaji wa Kiswahili Sanifu kama lugha ya pili; na kuibua mbinu zinazoweza kutumika katika kuzikabili athari za fonolojia ya Kihehe katika mawasiliano ya wajifunzaji wa Kiswahili Sanifu kama lugha ya pili. Utafiti huu ulifanyika nchini Tanzania katika Mkoa wa Iringa, Wilaya ya Kilolo, katika Shule za msingi za Lyamko, Boma la Ng’ombe, Ng’ang’ange na Mdeke. Huu ulikuwa ni utafiti wa kitaamuli na mbinu zilizotumiwa kukusanya data ni usimulizi wa hadithi, usaili, jaribio na uchambuzi matini. Ulihusisha sampuli ya watafitiwa (32) kwa mgawanyiko ufuatao: Wanafunzi (24) na walimu (8). Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa wajifunzaji lugha wa jamii ya Wahehe huiathiri lugha ya Kiswahili Sanifu kifonolojia kupitia uhawilishaji wa fonimu za Kihehe, yaani irabu /á:/ /é:/ /í:/ /ó:/ na /ú:/ zenye toni, na konsonanti /s/ /f/ na /l/, pamoja na viarudhi. Viarudhi vya Kihehe vilivyobainika kuhawilishwa ni toni, wakaa na lafudhi. Uhawilishwaji wa vipengele hivyo umebainika kusababisha mabadiliko katika baadhi ya fonimu za Kiswahili Sanifu yanayoathiri mawasiliano kwa sababu ya upotoshwaji na uharibifu wa maana za maneno yake. Utafiti huu pia umebaini sababu anuwai za utokeaji wa athari za fonolojia ya Kihehe katika mawasiliano ya wajifunzaji wa Kiswahili Sanifu kama lugha ya pili. Baadhi ya sababu hizo ni athari za lugha ya kwanza, na tofauti za mfumo wa fonolojia baina ya Kiswahili Sanifu na Kihehe. Kutokana na matokeo haya, inapendekezwa kuwa mbinu mbalimbali zitumiwe ili kuzikabili athari za fonolojia ya Kihehe katika mawasiliano ya wajifunzaji wa Kiswahili Sanifu kama lugha ya pili. Baadhi ya mbinu hizo ni: kuwapo kwa vitabu na maandiko mbalimbali ya Kiswahili, kuwapo kwa uchangamani mpana wa jamii tofautitofauti na wajifunzaji lugha ya Kiswahili.
Description
Keywords
Citation
Ngenzi, M. (2023). Athari za fonolojia ya lugha ya kwanza katika mawasiliano ya wajifunzaji wa kiswahili sanifu kama lugha ya pili: uchunguzi kifani kihehe, (Doctoral Thesis) The University of Dodoma.
Collections