Humanities
Permanent URI for this community
Browse
Browsing Humanities by Subject "Ajira"
Now showing 1 - 2 of 2
Results Per Page
Sort Options
Item Vionjo vya Fasihi ya kisasa ya Kiswahili katika nyimbo teule za Singeli(Chuo Kikuu cha Dodoma, 2018) Zahoro, SelandaTasnifu hii inahusu vionjo vya fasihi ya kisasa ya Kiswahili katika nyimbo teule za singeli. Malengo mahususi ya utafiti yalikuwa matatu: Mosi, kufafanua misingi ya nyimbo teule za singeli. Pili, kubainisha vionjo vya fasihi ya kisasa ya Kiswahili vilivyotumiwa katika nyimbo teule za singeli. Na, tatu, kutathmini athari za vionjo vya fasihi ya kisasa ya Kiswahili vinavyojitokeza katika nyimbo teule za singeli kwa jamii. Vionjo vya kisasa vya Kiswahili ni sifa zinazotumiwa katika tanzu mbalimbali za fasihi, zikiwemo ushairi, riwaya na tamthiliya. Singeli ni aina ya muziki wenye mapigo ya haraka haraka ambao umechukua vionjo vyake kutoka katika ngoma mbalimbali za asili za kabila la Wazaramo na muziki wa taarabu. Kutokana na uhaba wa tafiti na tahakiki zilizofanywa kuhusu nyimbo za singeli, utafiti ulikusudia kuziba pengo hilo. Utafiti ulitumia usanifu wa kifani uliojiegemeza katika mkabala wa kitaamuli. Data za utafiti zilikusanywa katika mkoa wa Dar es Salaam. Mbinu zilizotumika wakati wa ukusanyaji wa data ni udurusu wa maandiko, usaili na ushuhudiaji. Nadharia ya Usasa ilitumika kufanikisha mchakato wa utafiti. Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa, nyimbo za singeli zimejikita katika kutoa burudani kwa jamii, kutumika kama chanzo cha ajira na kuutambulisha muziki halisi wa Kitanzania. Aidha, nyimbo za singeli zimechochea kufifia zaidi kwa ngoma za asili za Kizaramo, kuchochea ufyosi katika jamii na kuhamasisha ngono. Pia, matokeo yameonesha kuwa, ngoma mbalimbali kutoka kabila la Wazaramo pamoja na taarabu vimechangia katika kuibuka kwa muziki wa singeli.Item Wahusika wa kimimi katika riwaya ya Kiswahili: mifano kutoka dunia yao na nyuso za mwanamke(Chuo Kikuu cha Dodoma, 2018) Ali, Haji BakarUtafuti huu ulilenga kuchunguza wahusika wa Kimimi katika riwaya za Said Ahmed Mohamed kwa kujikita katika miktadha ya utokeaji wa wahusika hao, namna wahusika wanavyojikengeusha na jamii; na sababu za wahusika kujikengeusha. Matumizi ya wahusika wa Kimimi hayajachunguzwa vya kutosha. Yumkini, hali hii inasababisha kutokufahamika miongoni mwa wasomaji na wahakiki wa kazi za fasihi. Kazi tulizozipigia mbizi kwa kina katika kuchunguza wahusika wa Kimimi ni riwaya ya Dunia Yao na Nyuso za Mwanamke. Utafiti ulifanyika maktabani. Maeneo yaliyotumika kukusanyia data ni Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Zanzibar. Hakuna data yoyote ya kitakwimu iliyotumika katika utafiti huu, bali tulitumia mbinu ya ufafanuzi. Uchambuzi wa data umefanyika kwa kutumia mkabala wa kisaikochanganuzi ambapo uchambuzi ulifanyika kwa mbinu ya ufafanuzi. Matokeo yanaonesha kuwa, riwaya ya Dunia Yao na Nyuso za Mwanamke zimetumia miktadha ya chimbuko la kifasihi, kisiasa, shereheni, kazini, kifamilia, mahakamani na mitaani.Pia, wahusika wamejikengeusha kwa kugomea chakula, kutojali, ukivuli, kutokata tamaa, kushiriki ngono, usasa, ulevi na uongozi bora. Sababu za wahusika kujikengeusha ni ukosefu wa ajira, utandawazi, ukombozi wa mwanamke, siasa, utamaduni, habari na mawasiliano na usomi. Utafiti uliongozwa na mkabala wa Saikochanganuzi.Mchango mpya ulioibuliwa na utafiti huu katika taaluma ya fasihi ni huu. Mosi, kuibuliwa kwa miktadha ambayo wahusika wa Kimimi wamesawiriwa katika riwaya ya Dunia Yao na Nyuso za Mwanamke. Pili, Kufafanuliwa sababu za wahusika kujikengeusha na jamii. Tatu, kuibuliwa kwa sababu za wahusika kujikengeusha ambazo ni ukombozi, siasa, utamaduni na usomi.