Master Dissertations
Permanent URI for this collection
Browse
Browsing Master Dissertations by Subject "Asili"
Now showing 1 - 3 of 3
Results Per Page
Sort Options
Item Asili ya wapemba kwa mtazamo wa isimu mandhari(Chuo Kikuu cha Dodoma, 2015) Hamad, Abdallah SuleimanTasnifu inahusu uchunguzi juu ya Asili ya Wapemba kwa Mtazamo wa tawi la Isimuj amii la Isimu Mandhari. Isimu Mandhari ni mkabala wa kiisimu unaoshughulikia vipashio vya lugha vinavyohusiana na eneo fulani la watumiaji wa lugha inayohusika. Huchunguza umaeneo ndani ya lugha fulani. Kwa mfano, kuchunguza msamiati wa lugha unaotumika katika eneo fulani. Kipashio kimojawapo cha lugha, yaani maneno ya kategoria ya nomino (majina) yanachukua nafasi kubwa katika mkabala huu. Majina yanatuwezesha kupambanua maeneo mbalimbali ya watumiaji wa lugha inayohusika. Majina yana taarifa nyingi ziwahusuzo watumiaji wa majina hayo. Majina huakisi mfumo wa maisha ya jamii inayohusika. Ni sehemu ya kipashio cha lugha kinachopokea mabadiliko ya haraka kulingana na maendeleo yanayofikiwa katika jamii. Hivyo, majina yanaweza kutumika katika kuchunguza asili na historia ya watumiaji wa majina hayo. Kazi hii ilitumia majina ya watu na majina ya maeneo katika kisiwa cha Pemba kuchunguza asili ya Wapemba. Wanaisimujamii wanaamini kuwa utambulisho wa mtu unaweza kubainika kutokana na vigezo anuai vinavyoonekana na visivyoonekana. Massamba na wenziwe (2009:46) wamemnukuu Tabouret-Keller (1989), wameeleza kuwa utambulisho wa mtu umefungamana na mambo mengi ya kijamii kama vile lugha, utamaduni, mila na desturi, mavazi, chakula, dini (imani mbalimbali), historia ya jamii, siasa na uchumi. Kigezo cha mahali alikozaliwa mzungumzaji kinapaswa kuzingatiwa wakati wa utambulisho. Matumizi ya majina ya familia, majina ya vitu na majina ya matukio yamebainishwa na Massamba na wenziwe (2009:52-56) kuwa ni vibainishi vya utambulisho wa mtu na jamii kwa ujumla. Buberwa (2011) amechunguza mofolojia (muundo) wa majina ya vituo vya daladala jijini Dar es Salaam kama sehemu ya majina mahususi ambayo haijashughulikiwa kwa nadharia za kimuundo. Miongoni mwa wataalamu waliobainishwa na Buberwa (2011) kuwa wamechunguza vipengele anuai kuhusu majina ni Allen (1945), Powicke (1954), Roden (1974), Brown (1975), Schotsman (2003), Angus (2005), Rugemalira (2005), Rye (2006), Majapelo (2009) na Rayburn (2010). Okal (2012) ameonesha jinsi majina ya watu yalivyowashughulisha baadhi ya watafiti. Imeelezwa kuwa majina huwa na dhima muhimu katika jamii. Data nyingi zilikusanywa uwandani. Maeneo tofauti ya kisiwa cha Pemba yalihusishwa. Mbinu ya awali tuliyoitumia katika ukusanyaji wa data ilikuwa ni ugawaji wa madodoso kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari za Pemba ili kutusaidia katika kuyatambua maeneo ya awali kukaliwa pamoja na maeneo yenye taarifa za kihistoria. Baadaye, mbinu ya mahojiano ilitumika. Ushuhudiaji pamoja na uzoefu wetu kwa maeneo ya utafiti viliturahisishia zoezi la ukusanyaji data na udhibiti wake. Mbinu ya udurusu wa maandiko ilitusaidia wakati wa kusoma kazi za waandishi mbalimbali. Data zilichambuliwa kwa mbinu ya maelezo kwa mwongozo wa nadharia ya Onomastiki. Uchunguzi wetu ulibaini kuwa majina yatumiwayo na Wapemba kama utambulisho wa mtu binafsi, ukoo wake au eneo analoishi yana taarifa nyingi kuhusu jamii inayohusika. Taarifa tulizozikusudia sisi ni zile zilizotuwezesha kufahamu asili ya jamii hiyo. Kupitia majina ya watu na majina ya maeneo tulibaini kuwa Wapemba ni watu wenye asili mchanganyiko baina ya Waafrika kutoka bara (Tanzania) na Waarabu (Washirazi) kutoka bara Arabu. Umuhimu wa matokeo ya utafiti huu unadhihirika kutokana na kuweka wazi hoja zilizoshindwa kupata mwafaka miongoni mwa watafiti waliotangulia kuhusu asili ya Wapemba. Tunaamini kuwa hitimisho la utafiti huu linakidhi mahitaji ya kitaaluma juu ya dhana iliyochunguzwa kwani taarifa zilizoelezwa humu zinahalisika.Item Ontolojia ya kiafrika katika mbolezi za wanyasa(Chuo Kikuu cha Dodoma, 2018) Kaponda, George JohnTasnifu hii inahusu Ontolojia ya Kiafrika katika Mbolezi za Wanyasa. Utafiti huu ulifanywa uwandani na maktabani ambapo uwandani, data zilikusanywa kwa kutumia mbinu za mahojiano, ushuhudiaji na mjadala wa vikundi. Kwa upande wa maktabani mtafiti alitumia mbinu ya udurusu maktaba.Utafiti uliongozwa na lengo kuu ambalo ni kubaini vipengele vya ontolojia ya Kiafrika katika mbolezi za Wanyasa. Malengo mahususi ambayo ni; kubainisha aina ya mbolezi zinazopatikana katika jamii ya Wanyasa, kubainisha vipengele vya ontolojia ya Kiafrika ya katika mbolezi za Wanyasa na kutathimini umuhimu wa ontolojia ya Kiafrika kwa jamii ya Wanyasa na Waafrika kwa ujumla. Utafiti uliongozwa na nadharia ya Ontolojia, mtafiti alikusanya mbolezi na dhana mbalimbali za ontolojia ya Kiafrika katika jamii ya Wanyasa. Jumla ya watafitiwa walioshiriki ni mia moja. Katika data zilizokusanywa, vipengele vilivyojitokeza vilijenga msingi wa data kuu iliyofanyiwa uchambuzi na kujadiliwa. Matokeo yanaonesha kuwa mbolezi zimegawanyika kulingana na vigezo vya chimbuko, rika na wakati. Katika chimbuko kuna mbolezi za asili na mbolezi changamani. Katika rika kuna mbolezi za watoto na mbolezi za watu wazima. Aidha, katika wakati kuna mbolezi za mara baada ya msiba kutokea, buriani, ibada ya mazishi na mazishi. Vipengele vya ontolojia ya Kiafrika vilivyobainishwa ni Mungu, ardhi, roho, kifo, mizimu na utu. Vipengele hivi vimebainika kuwa vimejengwa kiherakia na kutegemeana katika nguvu ijulikanayo kama kani uhai. Aidha, matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa jamii inaendelea kudumisha umoja na mshikamano, kurithisha amali, kulinda maadili, kutolea elimu na utambulisho wa jamii. Utafiti huu umependekeza tafiti nyingi zaidi ziendelee kufanyika kuhusiana na ontolojia ya Kiafrika katika fasihi simulizi.Item Semi zilizoandikwa katika maeneo ya biashara: uchunguzi kuhusu asili, muundo, miktadha ya utokeaji na dhima(Chuo Kikuu cha Dodoma, 2015) Shayo, Inocent FaustineTasnifu hii inatokana na utafiti uliofanywa kuhusu semi zilizoandikwa katika maeneo mbalimbali ya biashara. Mambo ya msingi yaliyochunguzwa katika semi hizi ni asili, miktadha ya utokeaji, miundo na dhima. Utafiti huu ulifanyika katika mji wa Same mkoani Kilimanjaro. Semi za biashara ni semi ambazo hujitokeza katika muktadha wa kibiashara kwa kuandikwa au kutumiwa katika mazungumzo ya kila siku ya kibiashara japokuwa utafiti uliangalia semi zilizoandikwa tu. Malengo mahususi ambayo yameuongoza utafiti huu yalikua manne ambayo ni: kubainisha semi mbalimbali zilizoandikwa katika maeneo ya biashara, kuchunguza miundo ya semi zilizoandikwa katika maeneo ya biashara, kuchunguza miktadha inayohusiana na kuibuka kwa semi zilizoandikwa katika maeneo ya biashara, pamoja na kuchunguza dhima za semi zilizoandikwa katika maeneo ya biashara. Nadharia ya Mwitikio wa msomaji ndiyo iliyotumika kuuongoza utafiti huu. Nadharia hii imetumika kwa sababu inahimiza juu ya mchango wa msomaji, mtazamaji au mwonaji wa kazi ya fasihi na sio mwandishi. Wauzaji, wamiliki na wateja wa maeneo mbalimbali ya biashara walihojiwa na kutoa maoni yao juu ya dhima na asili ya semi hizo. Hivyo, ili kufikia malengo ya utafiti huu nadharia hii ndiyo inayokidhi haja. Mbinu zilizotumika katika ukusanyaji wa data katika utafiti huu ni ushuhudiaji, udodosaji na maktabani. Vifaa vilivyotumika katika ukusanyaji wa data ni hojaji, kamera, ngamizi (kompyuta), shajara na simu. Utafiti umebaini kuwa semi zilizoandikwa katika maeneo mbalimbali ya biashara zimebeba dhima kubwa ambazo huielezea jamii katika nyanja zote yaani kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Vilevile, semi hizi huwa na miundo mbalimbali na hazitegemei muundo mmoja katika uandikwaji wake. Aidha, semi hizi hujitokeza katika miktadha tofauti tofauti kutegemeana na kusudio au dhima iliyobebwa. Utafiti huu umesaidia kuonesha na kutambulisha faida, umuhimu, na nafasi ya semi ambazo huandikwa katika maeneo ya biashara.