Semi zilizoandikwa katika maeneo ya biashara: uchunguzi kuhusu asili, muundo, miktadha ya utokeaji na dhima
Loading...
Date
2015
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Chuo Kikuu cha Dodoma
Abstract
Tasnifu hii inatokana na utafiti uliofanywa kuhusu semi zilizoandikwa katika
maeneo mbalimbali ya biashara. Mambo ya msingi yaliyochunguzwa katika semi
hizi ni asili, miktadha ya utokeaji, miundo na dhima. Utafiti huu ulifanyika katika
mji wa Same mkoani Kilimanjaro. Semi za biashara ni semi ambazo hujitokeza
katika muktadha wa kibiashara kwa kuandikwa au kutumiwa katika mazungumzo ya
kila siku ya kibiashara japokuwa utafiti uliangalia semi zilizoandikwa tu. Malengo
mahususi ambayo yameuongoza utafiti huu yalikua manne ambayo ni: kubainisha
semi mbalimbali zilizoandikwa katika maeneo ya biashara, kuchunguza miundo ya
semi zilizoandikwa katika maeneo ya biashara, kuchunguza miktadha inayohusiana
na kuibuka kwa semi zilizoandikwa katika maeneo ya biashara, pamoja na
kuchunguza dhima za semi zilizoandikwa katika maeneo ya biashara.
Nadharia ya Mwitikio wa msomaji ndiyo iliyotumika kuuongoza utafiti huu.
Nadharia hii imetumika kwa sababu inahimiza juu ya mchango wa msomaji,
mtazamaji au mwonaji wa kazi ya fasihi na sio mwandishi. Wauzaji, wamiliki na
wateja wa maeneo mbalimbali ya biashara walihojiwa na kutoa maoni yao juu ya
dhima na asili ya semi hizo. Hivyo, ili kufikia malengo ya utafiti huu nadharia hii
ndiyo inayokidhi haja.
Mbinu zilizotumika katika ukusanyaji wa data katika utafiti huu ni ushuhudiaji,
udodosaji na maktabani. Vifaa vilivyotumika katika ukusanyaji wa data ni hojaji,
kamera, ngamizi (kompyuta), shajara na simu.
Utafiti umebaini kuwa semi zilizoandikwa katika maeneo mbalimbali ya biashara
zimebeba dhima kubwa ambazo huielezea jamii katika nyanja zote yaani kiuchumi,
kisiasa na kiutamaduni. Vilevile, semi hizi huwa na miundo mbalimbali na
hazitegemei muundo mmoja katika uandikwaji wake. Aidha, semi hizi hujitokeza
katika miktadha tofauti tofauti kutegemeana na kusudio au dhima iliyobebwa.
Utafiti huu umesaidia kuonesha na kutambulisha faida, umuhimu, na nafasi ya semi
ambazo huandikwa katika maeneo ya biashara.
Description
Tasnifu (Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili)
Keywords
Semi, Biashara, Asili, Muundo, Miktadha, Dhima, Dhima za semi, Same, Kilimanjaro
Citation
Shayo, I. F. (2015). Semi zilizoandikwa katika maeneo ya biashara: uchunguzi kuhusu asili, muundo, miktadha ya utokeaji na dhima. Dodoma: Chuo Kikuu cha Dodoma