Nyimbo na Uchocheaji Mabadiliko ya Kijamii
Loading...
Date
2014
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Chuo Kikuu cha Dodoma
Abstract
Utafiti huu unahusu “Nyimbo na Uchocheaji Mabadiliko ya Kijamii”. Nyimbo
zilizotumiwa katika utafiti huu ni za BongoFleva zihusuzo UKIMWI. Utafiti umefanyika
katika mkoani Dar es salaam na Dodoma ambako data za uwandani na maktabani
zilikusanywa na kuchambuliwa kwa njia ya maelezo kwa sababu uchambuzi wake
haukuhusisha data za kitakwimu.
Malengo ya utafiti huu yalikuwa matatu, Mosi kubainisha nyimbo teule za BongoFleva
zinazohusu UKIMWI, ambapo nyimbo teule za BongoFleva zihusuzo UKIMWI
zimebainishwa. Pili, kuchambua maudhui yabebwayo na nyimbo teule zinazohusu
UKIMWI, ambapo nyimbo teule ishirini na mbili (22) za BongoFleva zihusuzo UKIMWI
zimechambuliwa. Hatimaye lengo la tatu lilikuwa kuchunguza jinsi maudhui ya nyimbo
teule za BongoFleva zihusuzo UKIMWI yanavyochochea mabadiliko katika jamii,
ambapo mabadiliko ya kijamii yameibuliwa na kufafanuliwa kwa njia ya maelezo.
Sampuli ya utafiti huu iligawanywa katika makundi mawili, kundi la kwanza lilihusisha
ukusanyaji wa nyimbo za BongoFleva zihusuzo UKIMWI ambapo jumla ya nyimbo
thelathini na nne (34) zilikusanywa na nyimbo ishirini na mbili (22) zilichambuliwa.
Kundi la pili lilihusisha jamii ya wasikilizaji, ambapo wasikilizaji arobaini (40) walipewa
dodoso kutoa taarifa za utafiti huu, kwa mgawanyo wa wasikilizaji wa uraiani (10),
wanafunzi wa Shule za Sekondari kumi na tano (15). wanafunzi wa Vyuo watano (5) na
walimu (10) ambapo makundi haya yalitoa taarifa zilizotumiwa katika mjadala wa utafiti
huu.
Uchambuzi wa utafiti huu umetumia nadharia ya Mwitiko wa Msomaji kama kiongozeo
cha kuyachunguza maudhui ya nyimbo za BongoFleva na uchocheaji wa mabadiliko ya
kijamii.
Nadharia ya mwitiko wa msomaji imetumiwa kutoa mwongozo wa namna hadhira au
mpokeaji wa kazi ya fasihi anavyotumia mazingira na uwezo wake, kupokea na kutafsiri
kazi ya fasihi. Ufafanuzi wa taarifa zote zilizochambuliwa umetolewa kwa njia ya
maelezo kutokana na utafiti kutohusisha taarifa za kitakwimu.
Matokeo ya utafiti huu yameonesha kuwa nyimbo za BongoFleva zihusuzo UKIMWI
zimebeba maudhui muhimu yenye mafunzo na maadili kwa mabadiliko ya jamii.
Mabadiliko yaliyobainika katika uchambuzi wa taarifa za utafiti ni pamoja na tabia,
mitazamo ya kiitikadi, saikolojia, na dhana potofu. Pamoja na mafunzo na maadili
yanayosanifiwa na nyimbo za BongoFleva zihusuzo UKIMWI, utafiti umebaini baadhi ya
watu kuvutiwa zaidi na ala za muziki na sauti za wasanii kuliko ujumbe wa nyimbo hizo.
Katika hitimisho la utafiti huu tumetoa mapendekezo kama: mosi, nyimbo zipewe
kipaumbele katika mapambano dhidi ya UKIMWI, ili kunusuru jamii hasa vijana dhidi ya
maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI. Pendekezo hili limetokana na ukweli
kwamba vijana hupenda sana nyimbo za muziki wa BongoFleva kwa sababu huwa zina
mvuto kwao na kwa upande mwingine vijana ndio wahanga wa maambukizi ya
UKIMWI. Pili, Jamii ielimishwe kutambua ufaafu wa nyimbo za BongoFleva katika
kueneza maudhui ya vita dhidi ya maambukizi VVU. Aidha, jamii zikubali kuweka kando
itikadi zinazopingana na ukweli juu ya maambukizi ya VVU, na kuchukua hatua ya
kushirikiana kwa pamoja kutokomeza maambukizi mapya ya VVU kwa jamii.
Description
Tasnifu (MA Kiswahili)
Keywords
Nyimbo, Ukimwi, BongoFleva, Dodoma, Fasihi, Maadili, Muziki, VVU, Mabadiliko kijamii, Dar es salaam
Citation
Ambilikile, A. (2014). Nyimbo na Uchocheaji Mabadiliko ya Kijamii (Tasnifu). Chuo Kikuu cha Dodoma, Dodoma.