Journal Articles
Permanent URI for this collection
Browse
Browsing Journal Articles by Author "Badru, Zuhura A."
Now showing 1 - 2 of 2
Results Per Page
Sort Options
Item Dhima ya taswira katika ufasiri na uteguzi wa vitendawili(Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 2019) Badru, Zuhura A.Vitendawili ni utanzu wa fasihi simulizi ambao umechunguzwa kwa kiasi kikubwa hasa kuhusu maana, muundo pamoja na dhima zake. Aidha, imedhihirika kuwa utanzu huu ni tajiri katika matumizi ya lugha ya picha na ishara ambazo hufumbata sitiari inayotarajiwa kufumbuliwa. Hata hivyo, namna ambavyo picha na ishara hizo hufasiriwa na kupata maana bado haijachunguzwa. Katika makala hii tumebainisha namna taswira zinavyowezesha vitendawili kueleweka kwa kurahisisha tafsiri ya picha zilizotumika, kuondoa utata, kutumia maneno kiiktisadi, na hivyo, kuwezesha hadhira kufumbua kitendawili kwa wepesi na kuuona ulimwengu wake kwa upya. Data za makala hii zilipatikana kwa njia ya uchunguzi matini, mahojiano na mjadala wa vikundi baina ya mtafiti na watoataarifa wake kutoka baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani. Imebainika kwamba taswira katika vitendawili ina dhima kadhaa katika ufasiri na uteguaji wa vitendawili hivyo, ikiwamo kuondoa utata, kuutazama ulimwengu upya na kuleta iktisadi.Item Taswira na mabadiliko ya kiujumi katika vitendawili vya kiswahili(Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 2020) Badru, Zuhura A.Kwa kuwa fasihi haitokei katika ombwe, haiwezi kuepuka mabadiliko ya kiutamaduni, kifalsafa na kiujumi. Makala haya yanaangazia suala hili kwa kujikita katika utanzu wa fasihi simulizi, hususan vitendawili. Vitendawili vya Kiswahili kama sehemu ya fasihi, haviepuki athari za mabadiliko ya kiujumi yanayoikumba jamii ambamo vimeundwa. Mtazamo wa mwandishi wa makala haya ni kuwa thamani ya kiujumi iliyokuwamo katika vitendawili vya wakati uliopita pamoja na taswira zilizotumika nyakati hizo zina tofauti kubwa na zilizomo katika vitendawili vya sasa. Kadiri ulimwengu halisi unavyobadilika, tunatarajia pia kuwa thamani ya kiujumi inabadilika na hivyo taswira zinazotumika katika vitendawili zinabadilika ili kuendana na hali hiyo. Mawazo haya ndiyo kiini cha makala haya ambayo yamejikita kwenye mjadala unaohusu taswira na mabadiliko ya kiujumi katika vitendawili vya Kiswahili. Makala yana jumla ya sehemu tano zilizopangwa kama ifuatavyo: Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambao unatoa picha ya jumla pamoja na kufafanua dhana za msingi kuhusu masuala yanayojadiliwa. Sehemu ya pili ni mapitio ya kazi tangulizi. Sehemu ya tatu inahusu methodolojia na nadharia ya utafiti. Matokeo ya uchambuzi yamebainishwa katika sehemu ya nne na sehemu tano ni hitimisho.